Get Even More Visitors To Your Blog, Upgrade To A Business Listing >>

Waziri Mchengerwa Azitaka Taasisi Za Kifedha Kutoa Mikopo Kupitia Hatimiliki Zinazotolewa Na MKURABITA

 


Na. James K. Mwanamyoto-Zanzibar
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezitaka taasisi za kifedha nchini kutoa mikopo kwa wananchi wenye hatimiliki za kimila zinazotolewa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) ili kuwawezesha wananchi hao kuendesha shughuli zao na kuinua kipato.

Akikabidhi hatimiliki hizo kwa baadhi ya wananchi wa Shehia ya Welezo, Zanzibar, Mhe. Mchengerwa amesema, hatimiliki hizo zinalenga kutoa fursa kwa wananchi kupata mikopo itayowawezesha kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo na biashara ili kuboresha maisha yao.

“Taasisi za kifedha zitambue hatimiliki hizi na kupunguza masharti ili kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kukopa na kuongeza mtaji.” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Akiwa katika kituo Jumuishi cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara kilichoko katika Baraza la Biashara, eneo la Darajani Wilaya ya Mjini, Mhe. Mchengerwa amezitaka pia taasisi za kifedha kutoa mikopo kwa wajasiriamali waliorasimisha biashara zao na kuongeza kuwa, mikopo hiyo itawaongezea mitaji ya kuendesha shughuli zao za ujasiriamali.

Kutokana na uwepo wa kituo hicho, Mhe. Mchengerwa amehimiza zoezi la urasimishaji biashara lisichukue muda mrefu ili kutoa hamasa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kurasimisha biashara zao.

Akieleza mchango wa ofisi yake katika zoezi la urasimishaji biashara, Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Dkt. Islam Seif Salum amesema kituo hicho kimejengwa ili kuondoa changamoto za urasimishaji walizokuwa wakikutana nazo wafanyabiashara wadogo.

Dkt. Salum ameongeza kuwa kutokana na faida za uwepo wa kituo hiki, Serikali imedhamiria kujenga kituo kama hiki Pemba ili wananchi wa eneo hilo nao waweze kunufaika.

Naye Mratibu wa Mkurabita, Dkt. Seraphia Mgembe amesema utekelezaji wa MKURABITA Zanzibar umewanufaisha wananchi wa Zanzibar kwa kuwapatia mafunzo ya utunzaji wa kumbukumbu za biashara ambapo hivi sasa wanazo takwimu sahihi za maendeleo ya biashara zao.

Mhe. Mchengerwa amehitimisha ziara yake ya kikazi Zanzibar ya kukagua miradi inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya ofisi yake ikiwa ni pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Sekretarieti ya Ajira ofisi ya Zanzibar.




This post first appeared on MASWAYETU, please read the originial post: here

Share the post

Waziri Mchengerwa Azitaka Taasisi Za Kifedha Kutoa Mikopo Kupitia Hatimiliki Zinazotolewa Na MKURABITA

×

Subscribe to Maswayetu

Get updates delivered right to your inbox!

Thank you for your subscription

×