Get Even More Visitors To Your Blog, Upgrade To A Business Listing >>

Ngeleja: Hakuna mgawo wa umeme

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja, amesema hakutakuwa na Mgawo wa Umeme mwaka huu.

Alitoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana alipokuwa akizungumzia ugunduzi wa gesi asilia katika eneo la Uyuni, Mashariki mwa Kisiwa cha Songosongo wilayani Kilwa.

Alisema ipo mikakati ya makusudi ya kuzuia kuwapo kwa hali hiyo nchini licha ya maji yaliyopo kwenye vyanzo mbalimbali vya nishati hiyo muhimu kutosha kwa kipindi hiki.

“Hakuna mgawo wa umeme, kwa sasa maji yapo ya kutosha katika mabwawa yetu…kwa hali hii hatuutarajii mgawo kwa mwaka huu kabisa lakini pia tuombe Mungu hali isibadilike.

“Hali ya maji, mipango na mikakati yetu ipo vizuri, napenda kuwahakikishia kuwa hakuna mgawo mwaka huu,” alisisitiza Ngeleja na kuongeza kwamba, serikali inajitahidi kuzuia hali hiyo kama ilivyotokea mwaka 2006.

Siku saba zilizopita, Mkurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), Idris Rashid, alikaririwa akitahadharisha kuwapo kwa mgawo wa umeme nchini.

Alisema kutokuwapo kwa mvua za kutosha ni moja ya sababu zitakazoleta mgawo wa umeme mwakani, licha ya shirika hilo kuhitaji sh trilioni 1.6 kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi.

Kuhusu gesi hiyo, alisema kampuni iliyoigundua ni Ndovu Resources Ltd kutoka Australia, yenye mkataba wa kutafuta mafuta ya petroli na gesi tangu Mei 19, mwaka 1999.

Alisema licha ya kugundua uwepo wa gesi hiyo, Kampuni ya Ndovu pia imechimba visima vitatu katika maeneo ya Uyuni, Kiliwani na Kiliwani North.

Alisema gesi hiyo iligundulika Machi 13 mwaka huu, kufanya visima vinavyotoa gesi nchini kufikia vinne katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwamo yanayopakana na Bahari ya Hindi. Pamoja na Uyuni, maeneo mengine yaliyogunduliwa gesi ni Songosongo, Mnazi Bay na Mkuranga.

Katika hilo, alibainisha kwamba kutokana na ugunduzi wa visima hivyo vya gesi, serikali inaokoa kiasi kikubwa cha fedha zilizotakiwa kutumika kwa kuagiza mafuta ya dizeli nje ya nchi kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli mbalimbali.

“Mfano katika mradi wa Songosongo kuanzia Juni 2004, gesi inayozalishwa inasaidia kutengeneza umeme kama nishati ya viwandani. Kiasi cha gesi kilichothibitishwa ni takriban futi za ujazo 540 bilioni.

Katika kipindi hiki taifa limeokoa dola za Marekani 992 milioni na vivyo hivyo katika mradi wa Mnazi Bay, ulioanza kuzalisha gesi ya ujazo wa futi 400 bilioni tangu Desemba mwaka 2006, umeokoa dola za Marekani 2.1 milioni,” alisema Ngeleja.

Mbali na hayo, alizungumzia mjadala wa wabunge kuhusu kukataliwa kwa muswada wa umeme na kufafanua kwamba, lengo si kubinafsisha Shirika la Umeme, badala yake ni kubadilisha sheria ya umeme ya mwaka 1931 ambayo imepitwa na wakati.

Aidha, aliitaka jamii ifahamu kwamba kupita au kutopita kwa muswada huo hakuhalalishi ubinafsishwaji wa TANESCO, na kuongeza kwamba wizara yake inaendelea kuufanyia marekebisho muswada huo.

Kuhusu dhana kwamba ipo faida inayopatikana kwa baadhi ya watendaji wa serikali ama wafanyabiashara, Waziri Ngeleja alikanusha na kusema uharakishwaji wa muswada huo unatokana na masilahi yake kwa jamii na taifa kwa jumla.

“Wapo baadhi ya watu wanadhani kwamba, kuna jambo nyuma ya pazia, lakini hakuna kitu, tunaipenda nchi yetu na tunafanya hivi kwa manufaa ya taifa kutokana na muswada uliokuwapo wa mwaka 1931 kupitwa na wakati. Mara zote unafanyiwa marekebisho lakini hayatoshi,” alisema Ngeleja.

Alisema, hivi sasa TANESCO linajiendesha kibiashara zaidi, hali iliyosababisha serikali kukatisha ruzuku kwa shirika hilo. Hivyo hata sheria ikipitishwa halitabinafsishwa.

Alisema: “Wizara inazingatia mapendekezo ya wabunge na itayafanyia kazi, lakini napenda wananchi waelewe kuwa Shirika la Umeme halitabinafsishwa na wala hakuna chochote nyuma ya pazia kuhusu muswada huu.”

Source: Tanzania Daima, 27/03/2008



This post first appeared on Godfreyenergy, please read the originial post: here

Share the post

Ngeleja: Hakuna mgawo wa umeme

×

Subscribe to Godfreyenergy

Get updates delivered right to your inbox!

Thank you for your subscription

×