Get Even More Visitors To Your Blog, Upgrade To A Business Listing >>

Haya ndio maisha wanayoishi waliobomolewa buguruni

DAR ES SALAAM: Huzuni! Mwishoni mwa wiki iliyopita, Zoezi la bomoabomoa ilifanyika Buguruni pembezoni mwa Reli ya Kati ambapo nyumba zaidi ya 200 zilibomolewa, lakini maisha ya waathirika wa tukio hilo ukiyaona ni lazima utoe machozi.
MAANDALIZI YA RELI:  Zoezi hilo linafanyika ikiwa ni maandalizi ya ujenzi wa reli ‘standard gauge’ kutoka Dar kuelekea Mwanza na Kigoma. Wanahabari wetu walikuta makundi ya watoto na akina mama wakiwa wamejikusanya hawajui pa kwenda baada ya makazi yao kubomolewa.
ULINZI WA POLISI: Wakati zoezi hilo likiendelea kufanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi wenye silaha, wakazi hao walipoteza mali nyingi, zikiwemo fenicha ambazo zilibebwa na vibaka waliojifanya wanatoa msaada. Wachache wao walifanikiwa kuokoa baadhi ya vitu kama vipande vya mabati, nondo, mbao na vinginevyo.
MALALAMIKO YA KUPOTEA MALI: Mwanamke mmoja aliyekataa kutaja jina lake, alisema amepoteza vitu vyake vipatavyo robo tatu ya alivyokuwa akimiliki, kwani vitu vyake vingi vilichukuliwa na watu ambao awali aliamini wanamsaidia, lakini wakapotea bila kujua walikoelekea.
“Nimepoteza fenicha, televisheni, vyombo vya ndani na fedha, zoezi hili ni uonevu kwa sababu mimi na familia yangu hatuna pa kulala wala kuishi, tunamuachia Mungu,” alisema mwanamke huyo. Kijana mwingine, Said Ali alisema yeye alikuwa mpangaji katika moja ya nyumba zilizobomolewa na wakati zoezi hilo linafanyika alikuwa kazini, hivyo kujikuta akipoteza vitu vyote vilivyokuwa ndani ya chumba.
“Ukweli ni kwamba nimepata hasara, vitu vyangu vyote vimepotea na katika zoezi kama hili utamuuliza nani?” alihoji kijana huyo huku akilengwalengwa machozi. Alisema alichoambulia ni godoro ambalo liliokolewa na mpangaji mwenzake kwani aliambiwa kulizuka vurugu kubwa wakati nyumba aliyopanga ilipokuwa inabomolewa. “Kwa kweli mambo kama haya yanasababisha wananchi kuichukia serikali,” alisema.
Naye Ashura Salum alisema walichofanyiwa ni unyama kwa sababu hakukuwa na sababu ya kulazimisha zoezi hilo kufanyika siku hiyo. “Wanasema wanataka kujenga reli ya kisasa, kwani itajengwa leo au kesho? Huku ni kutuonea,” alisema Ashura huku akifuta machozi.
AFANDE AFAFANUA: Mmoja wa askari aliyekuwa akisimamia zoezi hilo, aliyezungumza na Uwazi kwa sharti la kutotajwa jina, alisema: “Hawa wakazi leo unawaonea huruma, walishapewa notisi ya kuhama eneo hili karibu miezi mitatu iliyopita lakini wameendelea kuishi kwa ukaidi.
“Tulipima umbali wa mita 30 kila upande kutoka kwenye reli na kuweka alama nyumba zote zinazobomolewa na tukawapa notisi wahame, hivyo wasilalamike kuwa zoezi hili limefanywa kwa kuwashtukiza.”
SABABU ZA BOMOABOMOA: Zoezi hilo linaendelea kupisha ujenzi wa reli ya kisasa itakayokuwa na uwezo wa kuhimili mizigo yenye uzito mkubwa hivyo kuwepo usafiri wa treni utakaosaidia kupunguza foleni za malori hasa kwenye barabara ziendazo mikoani.This post first appeared on HABARI ZA SIASA NA MUZIKI, please read the originial post: here

Share the post

Haya ndio maisha wanayoishi waliobomolewa buguruni

×

Subscribe to Habari Za Siasa Na Muziki

Get updates delivered right to your inbox!

Thank you for your subscription

×