Get Even More Visitors To Your Blog, Upgrade To A Business Listing >>

ATHARI ZA KISUKARI KIPINDI CHA UJAUZITOUgonjwa wa Kisukari ni miongoni mwa maradhi sugu yanayoendelea kuathiri afya za mamilioni ya watu wa nchi nyingi duniani Tanzania ikiwamo.


Tunaelezwa kuwa kuna aina mbili za kisukari.  Aina ya kwanza huanzia utotoni, na madaktari hawajui jinsi ya kuizuia.  Lakini kuna aina ya pili ambayo imeathiri watu wengi kwa takribani asilimia 90 ya wanaougua ugonjwa huo.

Ingawa zamani aina ya pili ya kisukari ilihusianishwa tu na watu wazima, hivi karibuni imegundulika kuwaathiri pia watoto.

Lakini wataalamu wanasema mtu anaweza kujikinga ili asipatwe na kisukari.

Pamoja na kwamba ni tatizo kwa watu wengi wa rika na jinsia tofauti, ila kupanda kwa kiwango cha kisukari kumeweza kuwa tatizo pia kwa wajawazito kiasi cha kuwasababishia matatizo mbalimbali yeye na mtoto aliyeko tumboni.

Kisukari Cha Mimba kinawatokea hata wale ambao awali hawakuwahi kuugua ugonjwa huo.

Hali hiyo ikitokea humuweka mjamzito kwenye hatari ya kupata kifafa cha mimba, msongo wa mawazo pamoja na kujifungua kwa njia ya upasuaji.

Kisukari cha mimba huwakumba asilimia 3 hadi 9 ya wanawake katika ile miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito.

Huathiri asilimia moja ya wanawake waliochini ya miaka 20 na asilimia 30 ya walio juu ya miaka 44.

Asilimia 90 ya wanaokumbwa na tatizo hilo huweza kuondokana nalo baada tu ya kujifungua.

Utafiti unaonesha wanawake wenye kiwango kikubwa cha sukari kipindi cha ujauzito wapo katika hatari ya kujifungua watoto wakubwa, wenye kiwango kidogo cha sukari mwilini na wenye manjano.  Kisukari cha mimba ni hatari na kama hakitatibika, kinaweza kusababisha mtoto aliyeko tumboni kupoteza maisha.

Watoto wanaozaliwa baada ya muda kupita miezi tisa, huzaliwa wakiwa na uzito mkubwa na hupatwa na ugonjwa wa kisukari wakiwa na umri mkubwa.

Nini kinachochea kisukari cha mimba

Yapo mambo yanayochochea kisukari cha mimba ambayo ni pamoja na uzito wa kupindukia, historia ya kuwa na kisukari cha mimba katika ujauzito uliopita, historia ya ugonjwa wa kisukari hasa cha ukubwani katika familia, uvimbe katika ovari, hali inayofahamika kama polycystic ovarian syndrome, wanawake wenye umri juu ya miaka 35 wapo katika hatari.

Pia kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa katika ujauzito uliopita, matumizi ya dawa aina ya glucocorticoids na beta blockers au antipsychotics wakati wa ujauzito, huongeza hatari ya tatizo hilo, kuwa na kiwango kikubwa cha presha ya damu wakati wa ujauzito ni kichochezi pia.

Matatizo wakati wa ujauzito

Watoto wanaozaliwa na wanawake wenye kisukari cha mimba ambao hawakupatiwa matibabu, huwa na uzito mkubwa.

Lakini mjamzito aliyepatiwa matibabu ya tatizo hilo, mtoto anaweza akazaliwa mdogo ukilinganisha na miezi husika, kupatwa matatizo ya ukuaji akiwa ndani ya uzazi.

Utafiti unaonesha tatizo la kujifungua watoto wenye uzito mkubwa huwakumba wajawazito kwa asilimia 12.

Lakini wale ambao hawajawahi kuugua kisukari cha mimba wanaougua ni asilimia 20 pekee.

Hali ikoje upande wa watoto

Wale wanaozaliwa na mama zao wenye tatizo hilo, huwa katika hatari ya kuugua homa ya manjano na huwa na kiwango kidogo cha sukari, kiwango kikubwa cha chembechembe nyekundu za damu, kupatwa na matatizo katika mfumo wa hewa na kuathiri upumuaji kwa sababu ya kuzaliwa mapafu yakiwa bado machanga.

Pia huwa na kiwango kidogo cha madini ya kalisiamu pamoja na magnesium.

Mambo muhimu ya kuzingatia

Kuhudhulia kliniki mara kwa mara kutokana na maagizo ya daktari kunaweza kusaidia kulitatua tatizo hilo.

Mama anatakiwa kutunza afya yake kabla na baada ya kujifungua.
Anatakiwa ajitunze na ahakikishe kiwango chake cha sukari hakipandi kupitiliza hasa kwa wanawake wenye ugonjwa wa kisukari kabla ya ujauzito.

Wanatakiwa kuzingatia aina ya vyakula wanavyotumia, kufanya mazoezi na wazuie ongezeko la uzito.

Wanawake wenye mpango wa kubeba mimba na tayari wanaugua kisukari wanatakiwa kupata virutubisho vya folate hadi kipindi cha wiki mbili wakati wa ujauzito kusudi kuondoa hatari ya kujifungua watoto wenye matatizo kwenye mfumo wa fahamu yanayofahamika kama ‘neural tube defects’.

Kwa kuzingatia haya yote, itasaidia kuondoa matatizo kwa mama na mtoto kabla na hata baada ya kujifungua.This post first appeared on Afya Na Kiasi, please read the originial post: here

Share the post

ATHARI ZA KISUKARI KIPINDI CHA UJAUZITO

×

Subscribe to Afya Na Kiasi

Get updates delivered right to your inbox!

Thank you for your subscription

×