Get Even More Visitors To Your Blog, Upgrade To A Business Listing >>

SARATANI INAZIDI KUTEKETEZA MAISHA YA WANAWAKE



Februali 4 kila mwaka, dunia huadhimisha siku ya Saratani.  Siku hii hutumika zaidi kutoa elimu kwa umma juu ya madhara ya maradhi hayo na namna ya kukabiliana nayo na kauli mbiu kwa mwaka huu inasema, “Tunaweza, Ninaweza.”

Ujumbe huo umebeba dhana nzito kwani bado kuna dhana potofu imeendelea kujengeka miongoni mwa jamii juu ya maradhi hayo yanayoendelea kuathiri kwa kiwango kikubwa watu wengi duniani.
Tunaelezwa kuwa saratani ni miongoni mwa maradhi yanayoua watu wengi na hapa nchini hili linashuhudiwa.

Kwani jamii imeendelea kuwatesa hasa wanawake, mbali ya saratani ya shingo ya uzazi ipo ya matiti, na kwa wanaume saratani ya tezi dume imeendelea kugharimu maisha ya wengi wao.

Pia ndiyo ugonjwa ambao dawa zake zina gharama kubwa na kwa Tanzania, Serikali imeendelea kutumia mabilioni ya shilingi kukabiliana nao na kutibu walioathirika tayari.

Wataalamu wa afya wanasema saratani si ugonjwa mmoja bali ni mkusanyiko wa maradhi takribani 200 na kila ugonjwa ukiwa dalili zake tofauti na njia za kuupima na kuutibu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema viashiria vya kansa vitaongezeka kwa asilimia 70 katika kipindi cha miaka 20 ijayo.

Ugonjwa huo ni wa pili kwa kuua duniani kama ilivyoelezwa na mkurugenzi wa  Idara ya Kinga kutoka taasisi ya saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk Chrispin Kahesa.

Anasema watu milioni 6 hufariki duniani kila mwaka kutokana na saratani na wengi wao hutoka nchi zinazoendelea Tanzania ikiwa miongoni.

Je kwa Tanzania hali ikoje?

Dk Kahesa anasema ORCI hupokea wagonjwa wapya wa saratani 50,000 kila mwaka huku saratani ya shingo ya kizazi ikiongoza.

Anasema saratani ya shingo ya kizazi imekuwa tishio kwa wanawake wengi nchini.  Kwani takwimu za mwaka 2016 zinaonesha asilimia 33 ya wanawake wenye saratani, wanaugua saratani ya shingo ya kizazi.  “Wengi wao hupoteza maisha kutokana na kushindwa kubaini uwapo wa tatizo hilo,” anasema Mkurugenzi huyo wa Kinga na Tiba.

Anasema saratani ya shingo ya kizazi inashika nafasi ya pili kwa maradhi ya saratani kwa wanawake na ni sababu kubwa ya vifo vyao si kwa Tanzania tu, bali kwa nchi karibu zote zinazoendelea.
WHO inasema kama saratani hiyo haitachukuliwa hatua Zaidi, kuna uwezekano mkubwa ifikapo 2030 wanawake takribani 430,000 watafariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

Kwani kidunia, kati ya vifo 275,000 asilimia 85 husababishwa na saratani ya shingo ya kizazi.

Saratani hiyo husababishwa na nini?

Dk Kahesa anasema saratani ya shingo ya kizazi husababishwa na virusi vya HBV, HCV na Human papilloma Virus (HPV) vinasababishwa na ufanyaji wa ngono na hutokea zaidi katika nchi za Jangwa la Shara.  “Lakini kwa Tanzania kirusi cha HPV ndiyo chanzo kikubwa cha maambukizi ya saratani ya shingo ya uzazi,” anasema Dk Kahesa.

Anasema kama kinga ya mwili itashindwa kuondoa maambukizi ya virusi hivyo, ndipo mgonjwa huugua saratani ya shingo ya kizazi.

“Kama maambukizo hayo yataendelea kwa muda mrefu, chembe hai za kawaida huanza kukua bila mpangilio na kuwa saratani, jambo ambalo linaweza kuchukua miaka miwili hadi ishirini tangu kuambukizwa kuja kubainika,” anasema Dk Kahesa.

Anasema saratani nyingi wanazougua Watanzania zinasababishwa na virusi.  Anatolea mfano wa kirusi cha HPV ambacho huenea kwa njia ya kugusana sehemu za siri.

Anasema kirusi hicho huambukiza hata kama tendo la kujamiiana halifanyika.  Ili kujikinga na maambukizi hayo, Dk Kahesa anasisita matumizi ya mpira wa kiume ili kupunguza maambukizi lakini si kwa asilimia 100.  Dk Kahesa anasema kwa sasa maambukizi ni makubwa hasa kwa wanwake wenye umri chini ya miaka 25 ambao miili yao haijapambana na kupata kinga ya mwili ya kuviondoa virusi hivyo.

Kinachochangia maambukizi ya HPV

Baadhi ya vitu vinavyochangia maambukizi ya HPV ni kuanza kufanya tendo la kujamiiana katika umri mdogo, upungufu wa kinga mwilini, kurithishana kati ya vizazi na ukali wa virusi.  Dk Kahesa anasema hakuna dalili zinazojitokeza katika hatua za mwanzo za maambukizi, lakini katika hatua za mbele za ugonjwa, dalili zinazojitokeza kama kutokwa na damu au ute ukeni kusiko kwa kawaida, maumivu wakati wa tendo la kujamiiana, uvimbe ukeni na kutokwa haja ndogo na kubwa kusikojulikana.  Anasema upimaji wa ufasaha unawezesha ugunduzi wa mapema na huweza kuzuia kuendelea kwa ugonjwa na hatimaye kupunguza hatari ya vifo vitokanavyo na saratani hiyo.

Tatizo hilo linaweza kudhibitiwaje?

Anasema njia mbili za kuapambana na tatizo hilo ni kwa kupata chanjo dhidi ya virusi vya HPV.

Pia wanawake wanatakiwa kufanyiwa uchunguzi wa Mara Kwa Mara ili kugundua ugonjwa mapema.

Anasema tiba ya mapema ni gharama ndogo kuliko ile ya ugonjwa ulioenea na pia huweza kuondoa kabisa saratani.  Katika kukabiliana na saratani ya shingo ya uzazi, Dk Kahesa anasema tayari wameweka mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wa kike kuanzia darasa la nne nchini kote wanapatiwa chanjo itakayosaidia kuwakinga na saratani ya shingo ya kizazi.  “Wanaougua ugonjwa huu idadi yao ni kubwa lazima tuweke mikakati ya pamoja kuhakikisha  tunapunguza idadi hiyo, ni suala la kuamua tu kwa kuanzia na mtu mmoja mmoja, familia na mwisho kwa Watanzania wote na baadhi ya sababu zinazosababisha ugonjwa huu tunaweza kuzikwepa,” anasema.

Saratani ya matiti

Tofauti na maradhi mengine kama malaria ambayo dalili zake hueleweka, saratani ya matiti hushambulia kimya kimya.

Saratani ya matiti ni miongoni mwa inayokatisha uhai wa maelfu ya wanawake kila mwaka na ni ya pili kwa kusababisha vifo vya wanawake duniani kutokana na kutogundulika kwa wakati.

Saratani hiyo hutokea katika titi ambalo lina sehemu ya kutengenezea maziwa ijulikanayo kitabibu ‘Lobules na katika aina mojawapo ya mishipa inayounganisha yanapotengenezwa maziwa na chuchu.

Saratani hiyo inapotokea husababisha kubadilika kwa ukuaji wa chembe hai za mwili na kuwa wa kiholela pasipo kufuata utaratibu wa kawaida.

Sababu yake ni nini?

Bado sababu ya moja kwa moja inayosababisha saratani hiyo haijagunduliwa na wanasayansi na matibabu yake wanadai bado ni fumbo.  Lakini yapo mambo yanayoaminika kuchangia tatizo hilo ikiwamo aina fulani ya chembe za urithi inayosababisha chembe zingine zipoteze ufanisi wake.

Pia kuanza hedhi katika umri mdogo au kukoma siku katika umri mkubwa, kutozaa kabisa na kutonyonyesha kabisa au kunyonyesha kwa muda mfupi.

Tabia ya kutumia mafuta mengi kwenye chakula nayo ni miongoni mwa sababu, kutofanya mazoezi ya mara kwa mara, unene kupita kiasi, uvutaji wa sigara, utumiaji wa pombe kupita kiasi na historia ya saratani ya matiti katika familia.

Dk Kahesa anasema saratani hiyo inaweza kuwakuta pia wanaume.
Anasema kwa Tanzania hadi sasa ni asilimia moja tu ya wanaume waliougua saratani ya matiti.

Matibabu ya saratani

Dk Mark Mseti mkuu wa kitengo cha Bima cha ORCI anasema matibabu ya saratani yanategemea vitu vikubwa vitatu.

Moja ni kujua hatua ya saratani iliyofikia, hali ya ugonjwa na ridhaa ya mgonjwa kuhusiana na aina ya matibabu anayotaka kupatiwa.

“Lakini hapa cha msingi ni muhimu kujua kuwa maradhi ya saratani hayaambukizi na yanaweza kukaa mwilini kati ya miaka mitano hadi 10, ndipo dalili zake huanza kujitokeza wazi,” anasema Dk Mseti.  Anatoa wito kwa jamii kujitokeza hospitali kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara ili kama maradhi hayo yapo yaweze kutibiwa haraka.

“Saratani inatibika, watu wawahi uchunguzi mapema.  Ukiwahi unapona na utarejea kwenye maisha yako ya kawaida,” anasema daktari huyo.



This post first appeared on Afya Na Kiasi, please read the originial post: here

Share the post

SARATANI INAZIDI KUTEKETEZA MAISHA YA WANAWAKE

×

Subscribe to Afya Na Kiasi

Get updates delivered right to your inbox!

Thank you for your subscription

×