Get Even More Visitors To Your Blog, Upgrade To A Business Listing >>

USAFI WA KINYWA KWA MJAMZITO NI MUHIMU KWA AFYA YA MTOTO

usafi wa kinywa kwa mjamzito

Wanawake wote huwa na dalili tofauti kipindi cha Ujauzito, ukiacha zile za jumla.  Wapo wanaohisi kichefuchefu wakati wengine hutapika na baadhi wakishindwa kula baadhi ya vyakula.

Kadri ujauzito unavyoendelea kukua, mjamzito hushauriwa kuhudhuria kliniki ili kufuatilia maendeleo ya kiumbe kilichomo tumboni.  Hii husaidia kufanikisha uzazi salama kwa afya ya mama na mtoto mtarajiwa.

Jambo lililozoeleka ni wajawazito wengi kuhudhuria  na kupata vipimo vya jumla, wachache huwa wanafuatilia hali za Meno na kinywa.  Tahadhali ni kwamba ujauzito unaweza kusababisha matatizo ya afya meno na kinywa cha mama husika.

Kutokana na uwezekano huo, ni muhimu kumuona daktari wa kinywa na meno wakati wa ujauzito kwa ajili ya uchunguzi, ushauri au tiba pale itakapohitajika ndani ya muda huo.

Ni muhimu kuzingatia upigaji wa mswaki kwa kutumia dawa ya meno yenye madini na floridi mara Mbili Kwa Siku na kufanya flosi mara moja kwa siku.  Kutunza usafi wa kinywa chako huweza kusaidia afya ya mama na mtoto.

Kipindi cha ujauzito

Kuwa mjamzito kunaambatana na majukumu mengi ambayo humuandama mama bila kujali ni ujauzito wake wa ngapi.  Pamoja na hayo yote, utunzaji wa afya ya kinywa ni jukumu ambalo halikwepeki.

Ni vizuri kuzungumza na daktari wa kinywa na meno kuhusu namna nzuri ya kukitunza ili kutoathiri afya yako kwa muda wote wa ujauzito pamoja na kuchagua dawa nzuri za kutumia kufanya hivyo kila itakapohitajika.  Kupiga mswaki kwa dawa ya meno yenye madini ya floridi mara mbili kwa siku na kufanya flosi ni utaratibu ambao hautakiwi kuachwa.  Kama kutahitajika kubadili dawa kutokana na mabadiliko hayo, ifanyike hivyo lakini mfumo huo wa usafi uendelee kama inavyopendekezwa.

Muone daktari

Kwa wanawake wengi, kwenda kumuona daktari wa meno kisha kupata matibabu wakati wa ujauzito ni jambo salama.  Kitu muhimu kinachohitajika ni kutosahau kumueleza umri wa ujauzito husika.

Licha ya umri wa ujauzito, daktari atahitaji kufahamu dawa za meno unazotumia kila siku na matibabu ya magonjwa mengine yoyote unayotibiwa ili ajue namna nzuri ya kukuhudumia bila kumuathiri mtoto.

Mabadiliko ya kinywa

Wakati wa ujauzito baadhi ya wanawake huweza kupata ugonjwa wa kuvimba au fizi kutoa damu hivyo kuwa nyekundu na kuuma pia.  Unaweza kuzuia ugonjwa huu kwa kuhakikisha meno na kinywa vinakuwa safi kwa kipindi chote cha ujauzito.

Daktari wa kinywa na meno anaweza kupendekeza kufanya usafi mara nyingi zaidi ya mbili kwa siku zinazofanywa na watu wote ili kuidhibiti hali hii.  Unapoona mabadiliko yoyote mwilini wakati wa ujauzito, tafadhali muone daktari wa meno, hii ni kwa sababu hali hii isipotibiwa inaweza kuleta madhara zaidi.

Vyakula

Je, unajua kwamba meno ya mtoto wako aliye tumboni huanza kutengenezwa kuanzia mwezi wa tatu mpaka wa sita wa ujauzito? Hii ndiyo maana unahitaji virutubisho vya kutosha hasa Vitamini A, C na D, protini, pamoja na madini ya kalsiumu na fosforasi.

Wakati ni jambo la kawaida kwa mama mjamzito kupenda kula zaidi, kula vyakula vya sukari inaweza kuwa ni kukaribisha kuoza kwa meno.  Unapokula tafadhali tumia zaidi vyakula vyenye kiasi kidogo cha sukari na ambavyo vina virutubisho vyote muhimu kwa faida yako na mtoto aliye tumboni.


Vyakula kama vile matunda, mboga za majani na jibini ni muhimu na itakuwa vizuri kufuata ushauri wa daktari kuhusu aina ya vyakula unavyopaswa kutumia kipindi hiki.


This post first appeared on Afya Na Kiasi, please read the originial post: here

Share the post

USAFI WA KINYWA KWA MJAMZITO NI MUHIMU KWA AFYA YA MTOTO

×

Subscribe to Afya Na Kiasi

Get updates delivered right to your inbox!

Thank you for your subscription

×