Get Even More Visitors To Your Blog, Upgrade To A Business Listing >>

VITILIGO UGONJWA WA NGOZI USIOJULIKANA NA WENGI

vitiligo ugonjwa wa ngozi

Ngozi ni muhimu kwa kila binadamu, hivyo kuhitaji kulindwa ili isidhurike na kuuathiri mwili licha ya kuwapo kwa zaidi ya magonjwa 6,000 yanayoweza kuushambulia.

Yapo magonjwa ya ngozi ambayo yakimpata mtu hupona haraka na kuiacha ikiwa katika hali yake ingawa mengine ni ya kudumu na yakitibiwa huchukua muda mrefu kupona, hivyo kumkosesha raha mgonjwa.

Vitiligo au mbaraga ni moja ya magonjwa ya kudumu ya ngozi ambayo huwanyima uhuru waathirika kutokana na kuhofia kutengwa na jamii, ingawa wapo wachache walioikubali hali hiyo na kuishi kwa mafanikio.

Dk Zeinabbas Ladha anasema Ugonjwa Huu ni miongoni mwa maradhi yanayotokea baada ya kinga za mwili kujishambulia (autoimmune reaction) na kuathiri seli za melanocytes (melanini), zinazotengeza rangi ya ngozi na kusababisha mabaka meupe katika baadhi ya maeneo ya mwili.

Kila mtu huzaliwa na chembechembe za melanini, hivyo ngozi yake ama kuwa nyeupe au nyeusi na pindi zinaposhambuliwa ngozi hupoteza rangi yake halisi na kupata maambukizi ya ugonjwa wa vitiligo.

Anasema ugonjwa huu unaweza kutokea sehemu yoyote ya mwili na hausababishwi na bakteria wala vijidudu.  Wagonjwa wengi, anasema wanaathirika zaidi katika maeneo yanayopigwa na jua kama vile usoni, mikononi, maeneo ya shingo na sehemu nyingine za mwili ingawa unaweza ukajitokeza sehemu yoyote.

Kitabibu, ugonjwa huu hauhusiani na kitu chochote mwilini isipokuwa kushambuliwa kwa chembechembe za melanini zinazotengeneza rangi ya ngozi.

Anasema sababu nyingine ya kupata ugonjwa wa vitiligo ni urithi kutoka miongoni mwa ndugu wa familia moja.  Kwamba, mtu anayezaliwa kutoka kwenye familia ambayo imewahi kuwa na mtu mwenye ugonjwa huu naye anaweza akaugua.

Dalili

Tofauti na ilivyo kwa maradhi mengine, mgonjwa wa vitiligo hapati dalili zozote mfano maumivu, kuwashwa au homa bali huanza kuona mabaka meupe au madoa yakijitokeza katika ngozi yake.

“ugonjwa huanza kwa sehemu ya ngozi kupoteza rangi yake halisi na kuenea kwa mabaka meupe yanayoficha ngozi halisi,” anasema Dk Ladha.

Kwa baadhi ya watu, ugonjwa husambaa mwilini ingawa kuna baadhi ambao huweza kuchukua muda mrefu kusambaa mwilini.
“ugonjwa huu hautabiriki, leo unaweza kuja na mabaka machache lakini kesho ukasambaa.  Unaweza kuwa na baka upande mmoja lakini baada ya siku chache ukajikuta una mabaka karibu mwili mzima,” anasema Dk Ladha.

Vitiligo hauchagui umri wala jinsia na mara nyingi huwapata vijana ingawa uwezekano mkubwa ni kuwapata watu wenye umri kati ya miaka 20 mpaka 40.  Kwa mtu mwenye chembechembe za ugonjwa huu, mpaka anapofikisha miaka 40 tayari dalili zake zitakuwa zimeshajitokeza.

Kuhusu tofauti ya maradhi haya na watu wenye ualbino, anasema kuna uhusiano mdogo.  “Watu wenye ulemavu wa ngozi wanakosa kabisa chembechembe za melanini zinazoweza kuwapa rangi ya ngozi wakati wenye vitiligo huwa na upungufu kwenye baadhi ya sehemu za mwili,” anasema.

Athari

Anasema mara nyingi wagonjwa wa vitiligo wanaathirika kisaikolojia kutokana na kubaguliwa na jamii inayowazunguka kwa hofu ya kuambukizwa wakiamini kuwa nao jirani kunaongeza uwezekano huo.

Imani ya wengi itokanayo na kutofahamu ukweli wa vitiligo, anasema ndiyo inayoongeza unyanyapaa kwenye jamii kwa kudhani ugonjwa huu una chembechembe za ualbino, hivyo kutokana na imani za kishirikina.

Kutokana na vitiligo, mgonjwa ana uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya ngozi pindi akipigwa na mwanga wa jua hasa kwenye sehemu zilizoathirika jambo ambalo wanatakiwa kuwa makini nalo wakati wote.

Matibabu

Kwa sasa, anasema, ugonjwa huu hauna tiba ya uhakika bali zipo dawa za kupaka ili kuzuia kuendelea kusambaa kwake.

Dk Syriacus Buguzi anasema vitiligo ni kama saratani na njia pekee ya kukabiliana nao ni kuiondoa sehemu iliyoathirika, vinginevyo utaendelea kusambaa mwilini kadri mabadiliko kwenye seli husika yatakavyokuwa yakishamiri.

“Unaanzia kwenye kinga za mwili, hivyo hakuna namna ya uhakika kuongeza uthabiti wa kinga hizo,” anasema Dk Syriacus.
Pamoja na hayo yote, kuna njia ambazo mgonjwa wa vitiligo anashauriwa kuzitumia ili kuepukana na madhara yanayoweza kutokea ambazo zinahiusisha kujifunika sehemu alizoathirika zisipigwe na mwanga wa jua, kupaka dawa ya kuzuia mwanga wa jua kuharibu ngozi na utumiaji wa taa za ultraviolet light ambazo husaidia kufubaza madoa yaliyotokea.

Kwa watoto wa kike, utumiaji wa vipodozi husaidia kuficha maeneo yaliyoathirika na kuzuia ngozi isiendelee kudhurika.

Duniani

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Vitiligo ya Kimataifa (VR Foundation), zinaonesha zaidi ya watu milioni 65 ni waathirika wa ugonjwa huu duniani kote.

Mara nyingi wagonjwa wa vitiligo wamekuwa wanakata tamaa na wakati mwingine wakijifungia ndani, kufadhaika na msongo.

Mrembo na mwanamitindo wa kimataifa wa Canada, Challente Brown almaarufu kama Winnie Harlow, baada ya kuyatia masikio yake pamba na kutojali kinachosemwa na wanaomtazama amefanikiwa kutimiza ndoto zake licha ya kuwa na maradhi haya.

Lee Thomas, mtangazi wa Fox 2, kituo cha runinga nchini Marekani hulazimika kupaka vipodozi usoni ili kuweka mlinganiko wa ngozi yake hasa maeneo yanayozunguka macho, pua na masikio yaliyoathirika na vitiligo ili kuepuka kuonekana akiwa na rangi mbili mbele ya kamera za kituo hicho.

Mwanamuziki mkongwe duniani na mfalme wa pop, marehemu Michael Jackson amewahi kusemwa kuwa na maradhi haya mikononi na kadri miaka ilivyozidi kwenda ulikuwa ukisambaa mwilini mwake.

Jamii

Theresia Maganga (60) mkazi wa mtoni kijichi jijini Dar Es Salaam ambaye ni mgonjwa wa vitiligo akiwa na mabaka chini ya shingo, anasema alishangaa baada ya kuona hali hiyo inamtokea.

Anasema amekuwa akiulizwa maswali mengi kutoka kwa watu ambao kila mmoja akiongea lake juu ya ugonjwa huo na baadhi wakikaa nae mbali, wakidhani unaambukiza jambo ambalo linamnyima uhuru wa kuchangamana nao.

“Nalazimika kuvaa nguo zinazoficha eneo hili ili watu wasinishangae,” anasema Theresia.


Anasema alitumia gharama kubwa kutafuta dawa za kumsaidia kupona kabla hajafahamu kuwa hauna tiba, lakini bado hali iliendelea kuwa vilevile huku hofu ya kuathirika ikizidi kumjaa baada ya kuona dalili za madoa miguuni.


This post first appeared on Afya Na Kiasi, please read the originial post: here

Share the post

VITILIGO UGONJWA WA NGOZI USIOJULIKANA NA WENGI

×

Subscribe to Afya Na Kiasi

Get updates delivered right to your inbox!

Thank you for your subscription

×