Get Even More Visitors To Your Blog, Upgrade To A Business Listing >>

UTI INAEPUKIKA KWA KUFUATA KANUNI ZA AFYA


Ugonjwa wa UTI


Maambukizi ya njia ya mkojo au UTI ni tatizo linalowapata watu wengi hasa wanawake na kujirudia mara kwa mara.  Wanawake wamekuwa wakiugua bila kufahamu namna ya kupunguza tatizo hili.
Zipo njia rahisi ambazo zikifanyika zinaweza kusaidia kupunguza au kuzuia mwanamke kupata UTI mara kwa mara.  Moja ya njia ya kujikinga na ugonjwa huu ni kunywa Maji mengi kila siku, kwa mtu mzima mwenye uzito kuanzia kilo 72, anywe lita 1.5 mpaka mbili kwa siku.
Hii itamfanya apate haja ndogo mara kwa mara hivyo kutowaruhusu bakteria kujenga makazi kwenye njia ya mkojo.  Inashauriwa kuepuka kuubana mkojo Kwa Muda Mrefu, badala yake, hakikisha unakwenda haja ndogo kila unapohisi kufanya hivyo.
Kwa wanawake walio kwenye siku zao, wanashauriwa kubadili pedi mara mbili au mara tatu kwa siku.  Kuvaa taulo hizo za kike kwa muda mrefu hutoa nafasi kwa bakteria wanaosababisha UTI kusababisha maradhi hayo.
Kwa wanawake wa rika lolote, haitakiwi kujisafisha ukeni kwa sabuni zenye kemikali au kujipulizia marashi yoyote sehemu hizo hata kutumia pedi zenye kemikali kukata harufu.  Mambo haya yanaharibu kinga ya maeneo hayo.
Unapojisafisha baada ya kujisaidia anzia mbele kurudi nyuma kuepusha bakteria walio eneo la haja kubwa kuingia kwenye njia ya mkojo.  Zingatia hili kila unapojichamba.
Usafi wa choo ni kitu kingine muhimu.  Mwaga maji kabla ya kwenda haja na tumia maji safi kujisafisha sehemu za siri baada ya kumaliza.  Weka mazingira ya mwili wako safi ili kuepuka maambukizi haya.
Kwa wenye wenza wanashauriwa kuepuka kujamiiana kinyume na maumbile kwani chanzo cha ugonjwa huu ni bakteria walio kwenye njia ya haja kubwa.
Safisha uke kabla ya kushiriki tendo la ndoa na nenda haja ndogo baada ya kumaliza kujamiiana.  Kama kuna haja, tumia mipira yenye vilainishi au mafuta ili kupunguza michubuko ukeni ambayo uwepo wake ni mazalia ya vimelea.
Kausha uke kwa kitambaa safi na kikavu, vaa nguo za ndani zilizotengenezwa kwa pamba ili kutokana na uwezo wake wa kunyonya maji kirahisi.
Vaa nguo za ndani zisizobana mwili na kuepuka zinazobana au zilizotengezwa kwa nailoni au silki kwani hazinyonyi maji au jasho hivyo kutengeneza mazingira ya mazalia ya vimelea wanaosababisha UTI.
Oga maji yanayotiririka kwani husaidia kuondoa uchafu na vimelea kirahisi vilivyopo.  Ikitakiwa kutumia maji yaliyotulia, hakikisha unatumia chombo cha peke yako.  Hii huwa ngumu kwa wanaoishi kwenye jamii mfano wanafunzi lakini kwa kuzingatia afya, inabidi iwe hivyo.
Wajawazito wapo kweye hatari zaidi ya kupata maradhi haya hivyo ni vizuri kwao na kula lishe bora na mlo uliosheheni protini, mboga za majani na matunda ili kujenga kinga imara ya mwili.  Hilo lifanyike sanjari na kuzingatia usafi.
Wajawazito wanatahadharishwa kutokurupuka kutumia dawa kwa ajili ya kutibu UTI kwani si dawa zote ni salama kwao.  Inapotakiwa kufanya hivyo basi iwe kwa ruhusa ya daktari anayekutibu na kushauri dawa ambayo haitaathiri ujauzito ulionao.
Unapohisi dalili au viashiria vya awali, unashauriwa kwenda hospitalini kwa ajili ya uchunguzi, matibabu na ushauri.  Epuka matibabu ya kienyeji mtaani kutoka kwa watu wasio na sifa stahiki za kutoa matibabu ya binadamu.  Shikamana na matibabu ya wataalamu wa afya na usikatishe dozi.


This post first appeared on Afya Na Kiasi, please read the originial post: here

Share the post

UTI INAEPUKIKA KWA KUFUATA KANUNI ZA AFYA

×

Subscribe to Afya Na Kiasi

Get updates delivered right to your inbox!

Thank you for your subscription

×