Get Even More Visitors To Your Blog, Upgrade To A Business Listing >>

UDSM Kusomesha Wanaopatwa Majanga

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeanzisha utaratibu wa kuwasomesha Wanafunzi wasiojiweza kifedha, wakiwamo wanaoshindwa kulipia ada na malazi baada ya wazazi au wategemezi wao kufariki dunia.
Hayo yalielezwa na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Rwekeza Mukandala alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe ofisini kwake chuoni hapo jana.
Prof. Mukandala (64), alisema kuna wakati mwanafunzi hujiunga na chuo hicho na kujitegemea kwa ada na malazi, lakini katikati ya masomo wazazi au walezi wake wakafariki dunia, hivyo kushindwa kumudu gharama za elimu ya juu.
Kutokana na changamoto hiyo, alisema UDSM kupitia baraza lake la chuo imekuwa na utaratibu wa kuwasaidia wanafunzi hao wachache wanaopatwa na majanga hayo.
"Kunakuwa na wanafunzi wanakuwa na shida sana, labda alikuja anajitegemea, wazazi wake ghafla wanakufa, Chuo kupitia baraza lake kimekuwa na utaratibu wa kuwasaidia wanafunzi hao wachache wenye shida kubwa ya kujikimu juu ya maisha," alisema Prof. Mukandala.
Alisema baraza hilo liliamua kwa mwanafunzi halali ambaye ameshadahiliwa kila kitu na baadaye baadhi ya majanga yakamtokea katika maisha yake na kumuathiri kimasomo, ili asiathirike zaidi kwa kushindwa kupata chakula na huduma nyingine, chuo kitampa msaada.
"Haswa pale mwanafunzi anakuja analia, sijala, baba mama wamekufa, wengine wanakuja hapa wazazi wao wamekufa kwenye ajali, wengine wamepata matatizo mbalimbali," alisema na kufafanua zaidi:
"Huko nyuma tulikuwa na uwezo wa kuwasaidia kwa kutoa fedha zangu mfukoni, lakini kwa sasa chuo kina utaratibu uliopitishwa na baraza kwa kuwasaidia wanafunzi waliopata shida ambazo haziwezi kutafutiwa ufumbuzi kwa haraka na kwa muda mfupi."
Alisema fedha wanazopewa wanafunzi hao na chuo kikuu hicho kikongwe zaidi nchini ni msaada na hivyo hazirejeshwi na wahusika hawawekwi kwenye orodha ya watu wanaopaswa kurejesha Mikopo ya Bodi ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya Nipashe na mtaalamu huyo wa sayansi ya siasa:
SWALI: Usumbufu katika kupata mikopo ndiyo tatizo namba moja la wanafunzi wa elimu ya juu kwa sasa. Kwa uzoefu wako kama mkufunzi lakini pia kama mtawala, ni vigezo gani vinaweza kuwa mwarobaini na mkanganyiko uliopo?
Prof. Mukandala: Nchi nyingi duniani ikiwamo Tanzania zinatambua haja ya kutoa elimu kwa wananchi wake.
Serikali ya Tanzania kwa awamu mbalimbali imeliona hilo, kwamba baada ya matatizo mbalimbali yaliyokuwa yanajitokeza ikaleta sera ya mikopo, msingi wake ukiwa ni wanafunzi wapewe mkopo kisha watarejesha baadaye wakishahitimu.
Baada ya kuanzisha sera hiyo, kulikuwa na changamoto nyingi mojawapo ni wanafunzi waliokuwa wanahitaji mkopo kuwa wengi, huku fedha kuwagawia wanafunzi ziakiwa ni kidogo
Hapo mwanzo wa sera hiyo kulikuwa na tatizo kubwa la mchakato wa namna ya kuwapata wanafunzi halisi wenye shida ya mkopo.
Walengwa ambao ni watoto wa maskini na wasio na wazazi ndiyo walihitajika wapate mikopo. Hapo ndipo matatizo yakaanza, hapo ndipo kulikuwa na mtafaruku na kutoelewana na uzembe.
Kwa serikali ya awamu ya tano hatua zimeshachuliwa za kuongeza pesa. Pia serikali imeshapitia vigezo kuhakikisha wale walengwa ambao ni watoto wa maskini na yatima wanapata mikopo.
Kitu ambacho wananchi wanapaswa kufahamu ni kwamba, serikali haisaidii elimu kupitia utoaji wa mikopo tu. Kwa vyuo vya umma serikali inagharamia pia kulipa mishahara yote ya watumishi, majengo makubwa yote ya vyuo vikuu yanajengwa na serikali, aidha kupitia mikopo au pesa ya moja kwa moja.
Kwa mwaka uliopita vijana wengi walipata mikopo kwa kozi zilizopewa kipaumbele, hata zile ambazo hazikuwa katika kipaumbele wanafunzi wake walipewa mikopo kwa asilimia mbalimbali.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) nayo imefanya makusanyo kwa wadaiwa, hali itakayosaidia serikali kutoa zaidi mikopo kwa wanafunzi wengine.
SWALI: UDSM ndiyo chuo kikuu namba moja kwa ubora wa elimu ya juu nchini. Matatizo yanayozunguka elimu hiyo kwa sasa, ikiwamo usumbufu katika upatikanaji wa mikopo, yanatishia nafasi hiyo kwa kiasi gani?
Prof. Mukandala: Masuala ya uwezo wa kulipia gharama za masomo kwa wanafunzi ni changamoto iliyopo dunia nzima.
Hata kampeni za urais Marekani zilizofanyika hivi karibuni walikuwa wanazungumzia masuala ya namna ya kutoa elimu kwa watu binafsi na taasisi za serikali.
Chuo ni lazima kiwe na mkakati wa kukabiliana na tatizo hilo kwa kushirikiana na wadau wote serikali na vyama vya wanafunzi. Serikali wanatoa miongozo na vigezo, bodi ya mikopo wanatekeleza hilo.
Sisi kama uongozi wa chuo tunajaribu kufuatilia na kuhakikisha kwamba huo utekelezaji unakwenda vizuri na hakuna mtu anayeonewa na kila mtu anayestahili anapatiwa mkopo.
Kwa wanafunzi ambao wanajilipia wenyewe chuo kina utaratibu wa kuwawezesha kulipa kidogo kidogo, lengo likiwa ni kuwawezesha kumaliza masomo yao.
Imeandikwa na Gwamaka Alipipi na Sanula Athanas >>NIPASHE


This post first appeared on MASWAYETU, please read the originial post: here

Share the post

UDSM Kusomesha Wanaopatwa Majanga

×

Subscribe to Maswayetu

Get updates delivered right to your inbox!

Thank you for your subscription

×